NIDA Yashinda Makombe Matatu (3) Kwa Mpigo Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki ya Mwanza

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imezidi kungara kwa kupata tuzo 3 za ushindi kwenye Maonesho ya 14 ya Biashara ya Afrika Mashariki (East Africa Trade Fair) yaliyofanyika mkoani Mwanza.  NIDA imeibuka mshindi wa kwanza kati ya taasisi za Serikali na Mwonyeshaji Bora (Best Exhibitor) kati ya washiriki zaidi ya 300 kwenye Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki (East Africa Trade Fair) kutokana na kutoa huduma kwa jamii na kufanya shughuli kwa uhalisia (practically). Sambamba na kupata vikombe viwili kwa nafasi ya kuwa mshindi wa kwanza kwenye vipengele hivyo, (NIDA imetunukiwa pia kikombe cha 3 kwa kushika nafasi ya 3 katika ushindi wa jumla.

Bw. Raphael Manase amesema, Wananchi waliopata fursa ya kutembelea banda la NIDA kwenye maonesho ya 14 ya Biashara ya Afrika Mashariki wamefanikiwa kupata Namba za Utambulisho wa Taifa, kundi lingine wamesajiliwa pamoja na wengine kupewa elimu mbalimbali juu ya huduma za kumrahisishia mwananchi kupata taarifa za maendeleo ya Usajili ambapo mwananchi anaweza kuzitumia na kufahamu Namba ya Utambulisho wake kiganjani.

Kwa upande wake Bi Agnes Gerald, Afisa Habari Mwandamizi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), amesema NIDA ina jukumu la kusimamia ujenzi wa Mfumo Mkuu wa Taifa wa Utambuzi wa watu ambao unahifadhi taarifa sahihi za raia, wageni wakaazi na wakimbizi wenye umri wa miaka 18 na zaidi kielektroniki na hatimaye taarifa hizo zinatumiwa na taasisi za Serikali na sekta binafsi katika kutoa huduma kwa wateja wao kwa urahisi”. Umadhubuti wa mfumo huo na mchango wake mkubwa kwa taasisi mbalimbali katika kuwapunguzia gharama za utambuzi na kuwarahisishia utoaji huduma kwa kuweza kuwafikia wateja wengi kwa muda mfupi umekuwa kichocheo kimojawapo cha kupata ushindi huo wa kishindo.

Naye Afisa Msajili wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza Bw. Adili Moshi amewataka wananchi wanaofika banda la NIDA Kusajiliwa, kuhakikisha wanajaza taarifa zao kwenye fomu ya Usajili kwa usahihi na kwa kutumia kalamu ya wino mweusi, kuhakikisha fomu hiyo inagongwa muhuri na kusainiwa ili kuthibitisha makazi ya mwombaji na Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa anakoishi mwombaji pamoja na kuweka nakala za viambatisho kadhaa kama vile: Cheti cha kuzaliwa, Kadi ya Mpiga Kura, Leseni ya udereva, Cheti cha elimu ya msingi na sekondari, Namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), Pasipoti, Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, Kadi ya mfuko wa hifadhi ya jamii ili kuondokana na usumbufu wa kulazimika kurudi kwa mara ya pili.

Bw. Manase amehitimisha kwa kuwahasa wananchi kujitokeza mapema Kusajiliwa ili wamiliki Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) mkononi mapema hasa kundi la wafanya biashara kwani itawasaidia kukata TIN, leseni ya biashara, kusajili kampuni, kupata Pasipoti, kufungua akaunti ya benki, kukopesheka kirahisi kwenye taasisi za fedha n.k.

 

Watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wakifurahia kupata tuzo 3 za ushindi kwa mara moja, kwenye Maonesho ya 14 ya Biashara ya Afrika Mashariki (East Africa Trade Fair), yaliyofanyika mkoani Mwanza. Raphaeli Manase Afisa Msajili mkoa wa Mwanza na Bi. Agnes Gerald, Afisa Habari Mwandamizi wakipokea kombe wakiwa wameambatana na Bi. Pendo Kishoa, Afisa Msajili wilaya ya Nyamagana na Grace Mwitagula, Afisa Msajili wilaya ya Ilemela.

Bw. Abasi Iwodya akitoa ufafanuzi kwa mwananchi aliyetembelea banda la NIDA juu ya taratibu za kufuata ili aweze Kusajiliwa kwa lengo la kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Taifa(NIN).

Mwananchi akichukuliwa alama za kibaiolojia na Afisa Msajili Bw. Erick Sabbi Jimmy katika banda la NIDA, kwenye Maonesho ya 14 ya Biashara ya Afrika Mashariki (East Africa Trade Fair), yaliyofanyika mkoani Mwanza.

Afisa Msajili wilaya ya Ilemela Bw. Adili Moshi, akimpatia fomu mwananchi huku akimwelekeza juu ya namna inavyotakiwa kujazwa kwenye Maonesho ya 14 ya Biashara ya Afrika Mashariki (East Africa Trade Fair), yaliyofanyika mkoani Mwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu