NIDA Yawezesha Wakulima, Wavuvi na Wafugaji Kutambuliwa Kwenye Maonesho ya Nanenane

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), yashiriki maonesho ya 27 ya wakulima, wavuvi na wafugaji yanayoadhimishwa kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi, wilayani Bariadi mkoani Simiyu. Maonesho hayo yenye kauli mbiu ‘Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi’ yamelenga kutoa fursa kwa taasisi mbalimbali nchini za serikali na binafsi kutoa elimu hasa ya teknolojia wanazozitumia na namna zinavyoweza kuwasaidia wakulima katika kurahisisha utekelezaji wa majuku yao ya kila siku ya  kilimo, ufugaji na uvuvi.

Meneja Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Bi. Julien Mafuru ameeleza kuwa NIDA imeshiriki kwenye maonesho ya Nanenane mwaka huu ili kutoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ambao hawajawahi Kusajiliwa popote nchini kusajiliwa, waombaji kuangalia taarifa za maombi ya Usajili yalipofikia kwa waliokamilisha Usajili, Elimu juu ya namna ya kupata Nakala ya Kitambulisho cha Taifa kupitia tovuti ya NIDA (www.nida.go.tz), Matumizi ya Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) na Kitambulisho cha Taifa, kukusanya maoni ya wateja kwa lengo la kupata mrejesho juu ya huduma zetu, kutangaza njia zetu mbalimbali tunazotumia kuwasiliana na wananchi pamoja na kutangaza ofisi zetu za Usajili zilizopo katika kila wilaya nchini.

Bi. Mafuru ameeleza kuwa mwitiko wa wananchi ni mkubwa hasa kundi la watu ambao waliokamilisha Usajili siku za nyuma, wengi wamefika katika banda la NIDA  (Na. 7) kwenye viwanja vya Nyakabindi na kupatiwa namba zao za Utambulisho wa Taifa (NIN) kwa ambao zimeshatoka. Namba hizo zimewasaidia kutambulika na kuweza kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kama vile kusajili laini, kukata TIN, kufungua akaunti ya benki, kupata mkopo kwenye SACCOSS n.k.

Kwa Upande wake Bi Fatuma Odoyo, mkazi wa Bariadi ameishukuru Serikali ya awamu ya 5 kupitia NIDA kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia kutoa huduma za Usajili kwenye maonesho ya Nanenane kwani  kwa upande wake alikuwa hajafika kwenye ofisi za Usajili za NIDA kupata huduma hiyo. ’Ndani ya maonesho haya niliposikia matangazo kwenye redio kuwa NIDA wapo nikafika kwenye banda lao na kukamilisha Usajili kwani nahofia laini yangu ya simu kufungwa muda wa ukomo wa kusajili laini ya simu kwa kutumia alama za kibaiolojia ambapo wanatuhitaji tuwe na namba ya NIDA ukifika’ Bi Fatuma amesema.

Bi Careen Kuwite Afisa Msajili Mkoa wa Simiyu ameeleza kuwa wananchi hususan kundi la wakulima, wavuvi na wafugaji wanapotambuliwa katika mfumo wa Utambuzi unaosimamiwa na NIDA na kupatiwa Namba ya Utambulisho, kunawawezesha kupata huduma za kijamii kirahisi kama vile kupata ruzuku za pembejeo za kilimo, kusajili laini ya simu,  kujisajili kwenye vyama vya ushirika (kwa wakulima, wavuvi na wafugaji), kufungua akauti ya benki, kupata msaada wa TASAF unaotolewa kwa kaya masikini, hati miliki ya kiwanja na nyumba, hati ya kusafiria ya kielekroniki, kusajili biashara na kampuni BRELA, kukata leseni ya udereva, kukopesheka kirahisi kwenye taasisi za fedha, kupata mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi, kuomba ajira, malipo ya pensheni pamoja na huduma nyingine nyingi.

Akihitimisha Bi. Julien amewasihi wakulima, wavuvi, wafugaji na wananchi wote kiujumla kujitokeza Kusajiliwa kwa wingi ili kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) kwa wakati. Aidha ameeleza kuwa wananchi watakaoshindwa kutumia fursa ya Kusajiliwa kwenye maonesho haya ya 27 ya Nanenane wafike kupata huduma katika ofisi za Usajili za NIDA zilizoko katika kila wilaya nchi nzima wakiwa wamekamilisha kujaza fomu za Usajili zinazopatikana serikali za mitaa, kwenye tovti ya NIDA na kwenye ofisi za Usajili za NIDA.

 

Meneja Usajili Bi Julien Mafuru wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), akitoa maelekezo ya namna fomu ya Usajili na Utambuzi wa watu inavyojazwa kwa wananchi wa Simiyu waliofika kutembelea banda la NIDA kwenye maonesho ya 27 ya Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi vilivyoko wilaya ya Bariadi.

 

Bw. Humphrey Mwamba Afisa Msajili Msaidizi wilaya ya Bariadi, akiwaelimisha wanafunzi juu ya umuhimu wa wao Kusajiliwa na Kutambuliwa ili wanapohitimu masomo yao na kuhitaji kuendelea na ngazi ya juu wawe na Namba ya Utambulisho itakayowawezesha kukidhi vigezo vya kuomba mkopo wa elimu ya juu unaotolewa na Bodi ya Mikopo.

 

Bi Careen Kuwite, Afisa Msajili Mkoa wa Simiyu, akikagua fomu za Usajili za wananchi waliorudisha baada ya kukamilisha kuzijaza ili waruhusiwe kushiriki hatua ya pili ya kuchukuliwa alama za kibaiolojia kwa ajili ya kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Taifa kwenye maonesho ya 27 ya Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi vilivyoko wilaya ya Bariadi.

 

Meneja Usajili Bi. Julien Mafuru, aliyeketi wa pili kutoka kushoto katika picha ya pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa walioshiriki maadhimisho ya 27 ya  sikukuu ya wakulima (Nanenane) katika viwanja vya Nyakabindi wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *