Ninawapongeza kwa kuanzisha mfumo wa mtu kufuatilia taarifa za Kitambulisho cha Taifa kwa njia ya mtandao *152*00#

Habari za kazi waheshimiwa.

Ninawapongeza kwa kuanzisha mfumo wa mtu kufuatilia taarifa za Kitambulisho cha Taifa kwa njia ya mtandao *152*00#.

Kwa kweli hongera sana!

Pamoja na kwamba nimekutana na baadhi ya wananchi ambao ni wagumu kuelewa wakilalamikia Shilingi 100/- wanayokatwa kwenye sms ya majibu, lakini bado ni nafuu sana ukilinganisha na nauli ya daladala au boda boda ya kwenda na kurudi kwenye ofisi za NIDA ambayo haipungui Shilingi 1000/-.

Zaidi ya yote inaokoa muda ambao unautumia kutekeleza mambo mengine wakati umeshapata taarifa za hali au hatua ya Kitambulisho chako. Unapata taarifa kutoka NIDA bila kuondoka ulipo na bila kuacha majukumu.

Baada ya kupata taarifa kwa njia ya mtandao, inakusaidia kufahamu cha kufanya na wapi pa kuanzia na kuokoa muda wa kwenda na kurudi kuleta au kurekebisha hiki na kile.

Kwa mfano mimi nilikuwa nimeomba Kitambulisho wakati wa Saba Saba ya mwaka jana 2018 ambapo NIDA walikuwa wanatangaza lengo lao la kugawa vitambulisho 10,000 kwenye msimu huo wa maonyesho ya Saba Saba. Watu walikuwa wengi sana. Tuliambiwa tukimaliza mchakato tusubiri kutaarifiwa kwa njia ya simu wakati vitambulisho vitakapokuwa tayari.

Kwa kweli nilisubiri mpaka mapema mwezi huu wa Aprili 2019 nilipopata sms kwenye simu yangu ikisema: “Kufahamu Namba yako ya Kitambulisho cha Taifa, piga *152*00#, chagua 3, kisha chagua 2. Vinginevyo fika NIDA.”

Nilifurahi na kufarijika sana nilipofuata utaratibu huo na kupokea sms iliyosema: “Ombi lako la Kitambulisho linaendelea kushughulikiwa. NIN yako ni:1970 0607 1510 XXXXXXXX.”

Ijapokuwa mwaka wangu wa kuzaliwa ulikuwa umekosewa kidogo kwa kuandikwa mwaka 1970 badala ya 1976, hiyo haikuzuia furaha yangu na faraja niliyoipata ya kujua kwamba kitambulisho changu kiko tayari.

Leo tarehe 8/4/2019 niliweza kufika NIDA tawi la TEMEKE. Nilifika mapokezi nikaeleza shida yangu kwa afisa aliyekuwepo mapokezi, kwamba mwaka wangu wa kuzaliwa siyo 1970 bali ni 1976. Kwa utulivu na ukarimu akaingia kwenye kompyuta iliyokuwa mbele yake, akasema kweli kulikuwa na makosa ya uchapaji. Akaandika majina yangu akasema nenda kwenye chumba cha kuchukulia vitambulisho, huko utaeleza shida yako. Watakusikiliza.

Nilipoingia chumba cha kuchukulia vitambulisho niliwakuta wengine pia wakisubiri kupewa vitambulisho. Mara akaingia afisa wa kugawa vitambulisho, akaniita jina langu nikaenda kupokea kitambulisho. Nikafurahi sana kukipokea mikononi mwangu!

Lakini nikamwambia, mwaka wa kuzaliwa ulioandikwa wa 1970 siyo sahihi. Mwaka wangu wa kuzaliwa ni 1976. Akasema nirudi kwa afisa wa kwenye dawati la mapokezi. Nikarudi, akaniandikia kimemo kinachoonesha tarehe yangu ya kuzaliwa (07/06/1976) akaniambia rudi kwenye chumba cha kuchukulia vitambulisho mwambie, “ni sisi tuliokosea kwenye uchapaji.”

Nikarudi, nikafanya hivyo, yule afisa akasoma kile kimemo, akaingia kwenye kompyuta iliyokuwa mbele yake, akabofya bofya mara kadhaa, akaniambia nenda urudi baada ya mwezi mmoja na nusu.

Moyoni nikaanza kujaribiwa kwamba bora ningekichukua hivyo hivyo! Lakini busara na hekima ya kawaida ikakataa! Kwa sababu nyaraka zangu zote zinaonesha kwamba nimezaliwa tarehe 07 Juni, 1976; haiwezekani kitambulisho muhimu kama hiki kiwe na data ya tofauti! Moyo ukatulia, na kuridhika kusubiri mwezi mmoja na nusu kama alivyosema afisa!

Pia kulikuwa na mwingine ambaye kulikuwa kosa kwenye mwezi aliozaliwa, naye alikuwa akifuatilia vile vile.

Nilipofika getini, nikawauliza walinzi wanaoandikisha watu wanaofika pale mamlaka ya vitambulisho vya Taifa Temeke, kama kuna watu wengine wanaoleta taarifa kuhusu miaka yao ya kuzaliwa kukosewa. Wakasema ndiyo wapo wamewasikia wakisema hivyo, tena wengine wametokea wakisema majina yamekosewa. Basi nikaishia hapo, kwa sababu nilikuwa nimeanza kujiingiza kwenye upaparazi wakati halikuwa lengo langu la kufika pale!

Basi nikaondoka mwenye furaha sana, kwa sababu nimekishika kitambulisho changu mikononi mwangu, ila sikuondoka nacho. Ninasubiri kuondoka na kinachonesha mwaka wangu sahihi wa kuzaliwa.

Siyo sahihi hata kidogo kuwalaumu maafisa wa NIDA kwa sababu tunafahamu changamoto ya kushughulika na data. Mara nyingine kibinadamu inatokea kukosea unaposhughulika na data, hasa zinapokuwa za maelfu na mamilioni ya watu.

Ni matumaini yangu kuwa kama NIDA imeweza kubuni na kufanikiwa kurahisisha suala la kufuatilia na kufahamu namba ya kitambulisho kwa njia ya mtandao, ambayo tunaifurahia sana, hata njia ya kuondoa kabisa makosa machache ya miaka, miezi na majina kwenye vitambulisho vya taifa, inawezekana!

Ni ajabu kwamba watu wengi niliowakuta na walionikuta kwenye chumba cha kuchukulia vitambulisho ambao nilibahatika kuzungumza nao walisema wamepata taarifa za vitambulisho vyao kwa njia ya mtandao huo unaonifurahisha sana wa *152*00#. Tena na wao walikuwa wakiufurahia na kuusifia sana.

Hongera sana NIDA! Mmekuja vizuri sana mwaka 2019. Mmefuzu!

EBELY RUGEMA
MHARIRI MTENDAJI, GAZETI LA NYAKATI
0763 305 670

ASANTE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *