Maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi yaenda sambamba na uzinduzi wa Jengo jipya la kisasa la ofisi ya NIDA

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe Dkt Khalid Salum Mohamed amezindua jengo la ofisi ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wanaoishi Wilaya ya Kati Dunga – Tanzania Zanzibar.

Uzinduzi huo ulifanyika na kushirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zikiwemo Taasisi za Muungano.

Akihutubia kwenye sherehe hizo Waziri Dkt. Khalid Salum Mohamed amewataka wananchi na wadau muhimu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA); kuhifadhi na kutunza miundombinu ya Mfumo wa Taifa na Utambuzi kwani taarifa zinazopatikana katika mfumo huo zitasaidia kupata takwimu sahihi ambazo zitaimarisha  uchumi wa Nchi.

Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa juhudi zake za kuboresha mradi wa Vitambulisho vya Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kujenga Ofisi  za Usajili katika Wilaya mbalimbali nchini, na kusisitiza umuhimu wa Vitambulisho hivyo kwa wananchi, Kiuchumi, Kijamii na Kiusalama.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dkt. Arnold M. Kihaule amesema, zaidi ya asilimia 96.5 ya wananchi wa Zanzibar wameshaandikishwa na zaidi ya asilimia 90 tayari wameshazalishiwa vitambulisho vyao.

Dkt Kihaule amesema kukamilika kwa jengo la ofisi ya usajili wilaya ya Kati Dunga  limegharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Bil. 1.9 na kufanya mpaka sasa jumla ya kiasi cha Shilingi Bil 32 kuwa zimetumika katika kujenga majengo 13 nchi nzima ambapo kwa upande wa Zanzibar jengo hilo linakuwa ni la kwanza kukamilika katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya ofisi za usajili.

Pia ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mchango wake mkubwa ilioutoa ikiwamo upatikanaji wa viwanja na kupatiwa msamaha wa kodi mbalimbali (exemption) ambazo zimesaidia kukamilika kwa jengo hilo linalotarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 47,000.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imeahidi kuendeleza mikakati ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa Wananchi, ambapo katika  awamu ya pili ya Ujenzi itakayoanza hivi karibuni itakuwa na ujenzi wa ofisi zingine tatu kwa Unguja na Pemba.

Awamu ya kwanza ya ujenzi mbali na Tanzania Zanzibar; maeneo mengine yaliyopata majengo ya Ofisi ni mikoa ya Mwanza, Morogoro, Dar-es-salaam, Kibaha na Arusha.

Ujenzi wa Ofisi hizo umetokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Korea Kusini kupitia Benki ya Exim Korea.

Pichani ni Mkurugenzi Mkuu NIDA, Dkt. Arnold M. Kihaule akimkaribisha Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Dkt. Khalid Salum Mohamed wakati wa uzinduzi wa Jengo jipya la ofisi za Usajili Wilaya ya Kati Dunga.

Mtoto Munawar akimpatia mkasi mgeni rasmi Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi kwa ajili ya kukata utepe kuashiria ufunguzi wa Jengo jipya la NIDA litakalotumiwa na wananchi wa Wilaya ya Kati Dunga

Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo jipya la NIDA wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo hilo Wilaya ya Kati Dunga.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuzindua jengo jipya la NIDA Wilaya ya Kati Dunga.

Kaimu Mkurugenzi NIDA Zanzibar Bw. Hassan H. Hassan akielezea jambo kwa mgeni rasmi na ujumbe wake wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo la ofisi za NIDA. Kulia ni Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed (Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi), wa pili kushoto ni Mh. Mohamed Aboud (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais) na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Dkt. Arnold M. Kihaule.

Baadhi ya watumishi wa NIDA Visiwani Zanzibar wakiwa wenye nyuso za furaha wakati wa sherehe za uzinduzi wa Jengo la Ofisi za NIDA wilaya ya Kati Dunga.

Mkurugenzi Mkuu NIDA, Dkt Arnold M. Kihaule akiiwasilisha taarifa ya ujenzi wakati wa sherehe ya Uzinduzi wa Jengo la NIDA Wilaya ya Kati Dunga.

Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed akizungumza mbele ya wageni waliohudhuria sherehe ya uzinduzi wa Jengo la NIDA wilaya ya Kati Dunga.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi, Mh. Dkt. Khalid Salum Mohamed(katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa NIDA wakati wa Sherehe ya uzinduzi wa Jengo jipya la NIDA wilaya ya Kati Dunga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu