Mkurugenzi Mkuu NIDA aanza kwa kukagua shughuli za Usajili Kwenye Ofisi za Wilaya; Na Kuzungumza na wananchi

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) Dkt. Arnold M. Kihaule, ameenza kazi kwa kukagua utendaji wa ofisi za Usajili za Mkoa wa Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine amezungumza na wananchi na kutembelea ofisi ya Serikali ya Mtaa ambako huduma ya utoaji wa fomu na ugawaji wa Vitambulisho zinaendelea.

Katika ziara hiyo Dkt. Kihaule aliyekuwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa Mamlaka hiyo; amepongeza kazi nzuri inayofanywa na wafanyakazi wa NIDA na kusisitiza watumishi kuzingatia utoaji wa huduma unaozingatia viwango ili kuweza kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima kwa wananchi.

Aidha amewashukuru viongozi na Watendaji katika Serikali za Mitaa kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi kuhakikisha wanapata Vitambulisho vya Taifa na kuahidi kuendelea kuwapa ushirikiano katika kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa.

Dkt. Arnold M. Kihaule aliteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo akijaza nafasi iliyoachwa wazi na Ndg. Andrew W. Massawe aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Ajira na Walemavu.

 

 

 

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Dkt. Arnold M. Kihaule akiweka saini katika kitabu cha wageni ofisi ya Usajili wilaya ya Kinondoni wakati alipofanya ziara kukagua namna shughuli za Usajili zinavyofanyika kituoni hapo.

 

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA akikagua fomu ya mmoja wa wananchi waliojitokeza kusajiliwa. Kutoka kulia ni Bw Dickson Mbanga Afisa Usajili wilaya ya Kinondoni na katikati ni Bw. Alphonce Malibiche, Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji  Vitambulisho vya Taifa.

 

Mkurugenzi Mkuu NIDA akikagua sehemu ya kutunzia Vitambulisho vya Taifa katika ofisi ya Usajili wilaya ya Kinondoni. Kuli ni Afisa Usajili wilaya ya Kinondoni na wa kwanza kushoto ni Bw. Melkiory Ndofi Mkurugenzi wa Idara ya Fedha na Utawala.

 

Mkazi wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Gift Emmanuel Nkya (aliyevaa nguo nyeusi) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuo cha Biashara CBE, akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa NIDA alipotembelea kituo cha Usajili Kawe jijini Dar-es-salaam.

 

Mkurugenzi Mkuu wa NIDA (aliyevaa koti) akiingia kwenye ofisi ya Serikali Mtaa wa Mzimuni wakati wa ziara yake kukagua uendeshaji shughuli za Usajili Wilaya ya Kinondoni. Hapa alishuhudia utaratibu wa ugawaji fomu za Usajili wa Vitambulisho vya Taifa  kwa wananchi na utaratibu wa kugawa Vitambulisho vya Taifa kupitia ofisi za Watendaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *