Katibu mkuu wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi atembelea NIDA

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Jacob Kingu, amefanya ziara kwenye kituo Kikuu cha Uchakataji, Uzalishaji na Utunzaji wa Taarifa (Data Centre) kilichoko Kibaha mkoani Pwani na kukagua shughuli za uchakataji wa taarifa na uzalishaji wa Vitambulisho.

Pia meefanya mazungumzo na Menejimenti ya NIDA na kusisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya Uzalishaji kwa kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa mitambo ya kisasa haraka ili kuongeza nguvu ya Uzalishaji kufuatia asilimia kubwa ya wananchi kukamilisha hatua ya awali ya Usajili na uchukuaji alama za kibaiolojia.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu; Mkurugenzi wa Uzalishaji Ndg. Alphonce Malibiche ameeleza mpaka sasa Mamlaka imefikia hatua nzuri katika Usajili na uzalishaji wa Namba za Utambulisho na kazi kubwa iliyopo sasa niya uzalishaji ambao umekuwa ukienda taratibu kutokana na uwezo mdogo wa  mashine zilizopo kushindwa kuzalisha kadi nyingi kwa mara moja.

Hata hivyo amesema tayari Mamlaka ilishachukua hatia za kuagiza mashine mpya na za kisasa kusaidia kuongeza kasi ya Uzalishaji na tayari mchakato wa kumpata mzabuni umefikia hatua nzuri na pindi taratibu zitakapokamilika mashine hizo zitafungwa mara moja.

Meja Jenerali Kingu amepongeza jitihada kubwa na nzuri zinazofanywa na Mamlaka na kusisitiza umuhimu wa wafanyakazi kufanya kazi kwa uzalendo na uadilifu mkubwa huku akiielekeza Menejimenti kuangalia namna bora ya kulinda na kuongeza maslahi ya watumishi wake; ili kuongeza morali na ufanisi katika utendaji.

Mamlaka inaendelea na zoezi la kuwasajili wananchi nchi nzima na mpaka sasa imeshasajili zaidi ya wananchi mil 19.2 nchi nzima; na hadi kufikia mwezi Desemba 2018 imelenga kuwa imesajiliwa zaidi ya watanzania mil 22.

 

Meja Jenerali Kingu (kushoto mwenye Kaunda suti nyeupe) akisikiliza maelezo ya jinsi uchakataji wa taarifa unavyofanywa na maafisa wa NIDA alipotembelea kituo cha Uchakataji wa taarifa. Kulia ni Ndg. Alphonce Malibiche( mwenye tai nyekundu) Mkurugenzi wa Uzalishaji akitoa maelezo; na waliomzunguka ni baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya NIDA.

 

Watumishi katika kitengo cha Uchakataji wa taarifa wakiendelea na hatua za uhakiki wa taarifa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Meja Jenerali Jacob Kingu.

 

Meja Jenerali Kingu akikagua kazi inayofanywa na watumishi katika kituo cha Uchakataji wa Taarifa Kibaha mkoani Pwani.

 

Akiwa kwenye chumba za Uzalishaji akikagua shughuli ya Uzalishaji ianvyoendelea pamoja na kuuliza maswali mbalimbali kwa wasimamizi wa shughuli ya Uzalishaji.

 

Hapa akibadilishana mawazo na Mkandarasi wa Ujenzi wa kituo cha Uchakataji wa Taarifa Kibaha Mr. Kim(Mwenye tai ya bluu), akiwa amezungukwa na wakurugenzi na wakuu wa Vitengo wa Mamlaka.

 

Akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inayoundwa na Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na Meneja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Fomu za Maombi ya Utambulisho

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu