NIDA yazindua ugawaji Vitambulisho vya Taifa mkoa wa Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghirwa amezindua rasmi kuanza kwa zoezi la Ugawaji Vitambulisho kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro baada ya Usajili wa Mkupuo kumalizika kwa asilimia 82%.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa zoezi la Usajili na Utambuzi liloanza mwezi Octoba 2017 kwenye sherehe za uzinduzi wa zoezi hilo; mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bi. Rose Joseph amesema mkoa wa Kilimanjaro umekuwa mkoa wa nne (4) kitaifa kumaliza awamu ya kwanza ya Usajili Wananchi na kuanza kugawa Vitambulisho kwa wananchi waliokidhi sifa na vigezo vya uraia.

Amesema ugawaji wa awamu ya kwanza ya Vitambulisho vya Taifa utafanyika kwenye ofisi za Watendaji wa Mitaa na Vijiji wananchi walikosajiliwa ambapo zaidi ya vitambulisho 250,000 vitagawanywa huku hatua za mapingamizi, uchakataji na uzalishaji wa Vitambulisho vingine zikiendelea kwa Wilaya zote za mkoa huo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi; Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kippi Warioba amesema kukamilika Usajili wa Umma hakumaanishi wananchi hawataendelea kusajiliwa; badala yake kuwataka wananchi ambao hawajasajiliwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kwenye ofisi za NIDA zilizoko kila Wilaya kwani manufaa ya Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi ni makubwa na mengi, na iwapo mwananchi atakosa kuwa na hati hiyo muhimu atakwama kufanikisha mambo mengi na muhimu ya kimaendeleo ikiwemo kushindwa kushiriki katika masuala muhimu ya kitaifa.

Mkuu wa Mkoa huo amewataka Wakuu wote wa Wilaya mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha wanahamasisha wananchi na kufuatilia kwa karibu kuhakikisha wananchi wote wenye sifa za kusajiliwa wanasajiliwa na kupata Vitambulisho vya Taifa kabla wananchi hawajaanza kukwama kufanya shughuli zao au kukumbwa na msako kwa kwa kukosa Hati hii muhimu inayowatambulisha kama Raia.

Sherehe za uzinduzi wa zoezi la ugawaji Vitambulisho mkoa wa Kilimanjaro zimehudhuriwa na Viongozi wa Dini, Wafanya biashara, Viongozi wa kisiasa, wananchi, watu wenye mahitaji maalumu na vyombo vya habari; ambapo zaidi ya wananchi 20 wawakilishi wa makundi mbalimbali walikabidhiwa Vitambulisho vyao, huku wakuu wa Wilaya za mkoa huo wakikabidhiwa zaidi ya Vitambulisho 250,000 vya awamu ya kwanza.

 

Mhe. Anna Mghirwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akihutubia kwenye sherehe za uzinduzi wa kuanza kwa zoezi la ugawaji Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro. Katikati ni Katibu Tawala mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Aisha Amour na kushoto ni mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA Bi. Rose Joseph.

 

Baadhi ya makundi wawakilishi wa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wakifuatilia kwa karibu matukio wakati wa sherehe za Uzunduzi wa zoezi la Ugawaji Vitambulisho vya Taifa kwa wanachi wa mkoa wa Kilimanjaro. Sherehe hizo zilifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa mkoa huo.

 

Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghirwa akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kuanza kwa ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro. Kushoto ni mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA Bi. Rose Joseph na Kushoto ni Mhandisi Aisha Amour.

 

Mgeni rasmi mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro akimkabidhi Ndg. Evance Moshi Kitambulisho chake kwa niaba ya kundi la watu wenye mahitaji maalumu

 

Mwakilishi wa kundi la viongozi wa dini Sista Eliaichi Malisa akikabidhiwa Kitambulisho chake na mgeni rasmi Mhe. Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro wakati wa sherehe za uzinduzi

 

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghirwa akibadilishana mawazo na mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA –  Bi. Rose Joseph (kulia)

 

Baadhi ya washiriki wa sherehe za uzinduzi wa zoezi la Ugawaji Vitambulisho vya Taifa mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye picha ya pamoja nje ya jengo la ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Leave a Reply to Andrew Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *