Utoaji nambari za Utambulisho wa Taifa kwenda sambamba za zoezi la usajili na uhakiki wa taarifa

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Ndugu Andrew W. Massawe amesema zoezi la utoaji nambari za Utambulisho wa Taifa kwa wanachi waliosajiliwa wakati wa uchaguzi 2015, litakwenda sambamba na usajili mpya kwa wale ambao hawakuwahi kusajiliwa, uhakiki wa Taarifa na kukamamilisha Usajili kwa wale waliokwisha sajiliwa.

Hayo ameyasema wakati wa ziara yake ya  kikazi aliyoifanya mkoani Arusha alipotembelea shughuli za Usajili na uchakataji wa Taarifa za Watumishi wa Umma zinazoendelea mkoani humo, pamoja na kukagua viwanja vya ujenzi wa ofisi za NIDA katika Wilaya za Arusha, Arumeru na Longido ujenzi unaokusudiwa kuanza hivi karibuni. Katika ziara hiyo alipata fursa ya kupokea taarifa za usajili katika kila Wilaya na kufanya mazungumzo na watendaji.

Akizungumzia mafanikio ya zoezi la Usajili wa Watumishi wa Umma lililokamilika hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi huyo amefurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi hao na kuwataka kuendeleza moyo wa uzalendo waliouonyesha katika kusimamia zoezi hilo.

“ Nimefurahishwa sana kuona Mkoa wa Arusha mmefanikiwa kukamilisha zoezi la Usajili wa Watumishi wa Umma kwa zaidi ya asilimia 95, pamoja na changamoto mbalimbali zilizokuwepo. Nawapongeza sana na hasa uongozi wa Mkoa  wa Arusha kwa jitihada kubwa za kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa kiwango hiki ” alisisitiza

Mbali na kusajili Watumishi wa Umma kwa sasa mkoa huo uko katika maandalizi ya kuanza kuwasajili na kuhakiki taarifa za wananchi wanaoishi mkoani humo ili nao kupata Vitambulisho vya Taifa, sambamba na kuanza usajili wa wageni wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wanaoishi kihalali mkoani humo.

Akisoma taarifa ya mkoa wa Niaba ya Afisa Usajili Mkoa (RRO), Ndugu Edward Bujune Afisa Usajili Wilaya ya Arumeru (DRO); amemwambia Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwa sasa Mkoa unakamilisha hatua ya uchakataji wa taarifa za Watumishi wa Umma baada kuendesha zoezi la Mapingamizi na tayari taarifa zimeshaanza kutumwa makao makuu katika kituo kikuu cha uzalishaji na muda si mrefu wataanza kugawa vitambulisho kwa baadhi ya watumishi ambao vitambulisho vyao vitakuwa tayari.

Alielezea changamoto za Usajili, ndugu Mujune amesema changamoto kubwa ilikuwa ni kupata usafiri kwa baadhi ya maeneo kwani  baadhi ya maeneo ni mbali na miundombinu ni mibovu hususani barabara na hivyo kulazimika kupoteza muda mwingi kutafuta mbinu mbadala za kuwafikia wananchi katika maeneo hayo.

Changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi kushindwa kuelewa umuhimu wa kuwa na vitambulisho vya Taifa, baadhi kuchanganya zoezi la Usajili wa Vitambulisho vya Taifa na Uhakiki wa taarifa za watumishi kiasi cha kufanya baadhi kushindwa kushiriki kwa hofu. Hata hivyo kwa kushirikiana na Uongozi wa mkoa walifanikiwa kutatua baadhi ya changamoto.

Kaimu Mkurugeniz Mkuu amewapongeza watumishi wote katika Mkoa wa Arusha, na kuwataka watumishi wote wa Mamlaka kuendelea kujibidisha katika kazi “Nichukue fursa hii kuwafikishia salamu watumishi wote wa Mamlaka kujizatiti zaidi katika kazi kwani kazi ndiyo msingi wa maendeleo” alisisitiza

Amesema kutokana na changamoto ya baadhi ya Taarifa za wananchi zilizokusanywa awali kutokidhi viwango vya NIDA, kuanza kwa utoaji wa nambari za Utambulisho wa Taifa (NIN) kutakwenda sambamba na ukusanyaji wa taarifa zinazokosekana ili kukamilisha usajili kwa kila mwombaji, pamoja na kufanya usajili wa wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa kabisa. Usajili wa wanachi umepangwa kuanza mapema mwakani na kwa kuanza utaanza kwa baadhi ya mikoa ukiwemo mkoa wa Arusha na kwamba NIDA itajitahidi kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa haraka na kwa muda mfupi ili kutoa fursa kwa wananchi kuanza kunufaika na Utambulisho wa Taifa.

Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa Mikoa ya Tanzania iliyoshiriki katika usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa Umma nchi nzima zoezi lililoanza Octoba 03 na kumalizika tarehe 31 Octoba 2016. Katika zoezi hilo zaidi ya watumishi 500,605 walisajiliwa nchi nzima.

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Bwana Andrew W. Massawe akiweka saini katika kitabu cha wageni mara baada ya  kuwasili katika Ofisi ya Usajili mkoa wa Arusha  wakati wa ziara ya kutembelea shughuli za Usajili na Utambuzi wa Watu katika Ofisi za Wilaya mkoani humo pamoja na viwanja vya ujenzi wa ofisi za kudumu za Usajili.

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, akizungumza na wafanyakazi katika ofisi ya usajili ya Wilaya ya Arusha na makao makuu ya mkoa wa huo ambapo shughuli za Usajili na Utambuzi zimekuwa zikifanyika.

 

Afisa Usajili- DRO  wa (kwanza kushoto) akiwasilisha kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu,  taarifa ya utekelezaji majukumu ya usajili mkoa wa Arusha kwa niaba ya Afisa ya Usajili mkoa. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu na wa mwisho kulia ni Kaimu Mkurugenzi Uzalishaji wa Vitambulisho vya Taifa, Bwana Alphonce Malibiche.

 

Wakiwa na furaha katika picha ya pamoja ni wafanyakazi wa NIDA Wilaya ya Arusha wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wakati alipofanya ziara ofisini hapo.

 

Meneja mradi wa ujenzi Bwana Alphonce Malibiche ( mwenye vazi jeusi) akitoa ufafanuzi wa mpango wa ujenzi wa ofizi za NIDA makao makuu ya mkoa wa Arusha kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu alipotembelea viwanja kwa ajili ya ujenzi utakaoanza hizi karibuni.

 

Watumishi katika Ofisi ya Wilaya ya Arumeru wakiwa tayari kumsikiliza Kaimu Mkurugenzi MKuu Bwana Andrew W. Massawe alipowatembelea.

 

Katika picha ya pamoja ni watendaji katika Ofisi ya Wilaya ya Arumeru na Kaimu Mkurugenzi Mkuu (Mwenye suti katikati). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Usajili bwana Alphoce Malibiche,  kulia ni Afisa Usajili wa Wilaya ya Arumeru Bwana Edward Mujune. Wengine ni watendaji katika ofisi hiyo.

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Nida akiwa na Mkandarasi wakikagua kiwanja cha ujenzi wa ofisi ya Wilaya ya Arumeru

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu akiwa tayari kuzungumza na watumishi katika Ofisi ya usajili ya Wilaya ya Longido alipofanya ziara kukagua shughuli za usajili.

 

Katika picha ya pamoja ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu NIDA (mwenye suti kati kati) na watumishi katika ofisi ya Usajili ya Wlaya ya Longido mkoani Arusha alipofanya ziara kutembelea kuona shughuli za Usajili. Kulia ni Afisa Usajili Wilaya ya Longido bwana Emmanuel Tarimo, kulia ni kaimu Afisa usajili bwana Elisha Pununta, akifuatiwa kulia na bwana Alphonce Malibiche, Jerome Rugo na kulia bwana Edward Bujune.

 

Bwana Jerome Rugo wa Idara ya Mipango, Bajeti na Mipango (NIDA) akifafanua kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu (Katikati) mgawanyo wa eneo la ujenzi wa Ofisi ya Wilaya Longido. Wengine katika picha ni wawakilishi upande wa Mkandarasi Mkuu na Mkandarasi ujenzi .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Namba za vitambulisho zilizotengenezwa

Tarehe idadi
10 August 2016 (....)

Ukurasa wetu wa Facebook

Ramani ya Ofisi Zetu